Monday, January 11, 2016

Workshop of cameramen

 Baada ya mafunzo ya nadharia sasa ni vitendo....
(Pichani ni; kwenye kamera ni Abubakar Kondo, katikati ni Khaleyd Juma na pembeni kushoto ni Madebe Lidai)

Tuesday, June 19, 2012

MPANGO WA SERIKALI KWA WASANII NI MAZINGAOMBWE!!

Naongelea ninalojijua, tasnia ya filamu.

Mimi ni mdau wa filamu kutokana na kuwemo katika tasnia kwa zaidi ya miaka kumi kama Mwongozaji (Director), Mwandika mswada (scriptwriter), Mtayarishaji (Producer) na Mkuu wa sakafu (Production Manager) katika filamu zaidi ya ishirini na tano zikiwemo AUGUA (2001), FIKIRI (2004), SANDA NYEUSI(2008), BESTMAN (2009), WRONG DECISION (2010), ASALI CHACHU (2010) na DIANA (2012).

Pia nimekuwa mwanaharakati katika maendeleo ya tasnia ya filamu kwa muda wote huo zikiwemo harakati za kutoa mafunzo kwa waigizaji DDC Magomeni Kondoa (2000 - 2004), Mafunzo ya uandishi wa miswada katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (2007) na harakati za mchakato wa marekebisho ya sheria ya filamu na uanzishwaji wa shirikisho la filamu kupitia Bodi ya Ukaguzi wa Filamu (2009).

Usimamizi wa tasnia ya filamu
Hadi muda huu sheria inayosimamia tasnia ya filamu ni Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya mwaka 1976 ambayo iliunda Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza.

Hata ilipoundwa sheria namba 23 ya mwaka 1984 iliyoanzisha BARZA LA SANAA LA TAIFA (BASATA) kwa kuunganisha Baraza la Sanaa la Taifa na Baraza la Muziki la Taifa na kuitambua Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa ya mwaka 1974, haikuifuta sheria ya filamu na michezo ya kuigiza ya 1976 wala haikuwa na lengo la kuipa BASATA nguvu ya kusimamia filamu kama wanavyojaribu kufanya hivi sasa.

Pamoja na tafsiri nyingine za kazi za sanaa katika sheria iliyounda Basata kipengele cha 2(a)(iv), kazi ya sanaa inayosimamiwa na BASATA imetafsiriwa kama 'Picha ambazo hazikutengenezwa kwenye mashine ya picha za filamu'

Filamu ni zaidi ya sanaa, ni suala mtambuka ambalo linahusisha taaluma nyingi, na waigizaji ambao ni wasanii ni sehemu ndogo tu ya tasnia ya filamu ila huwa wanaonekana kuwa na nguvu sana kwa kuwa ndiyo wanaoonekana. Wasanii wengine katika tasnia ya filamu ni wabunifu wa mavazi, warembaji na wapambaji wa sehemu za kuchukulia picha.

Kwa kuwa wakati inatengenezwa sheria hiyo ya Filamu na Michezo ya kuigiza ya mwaka 1976 hakukuwa na televisheni, wasambazaji wala maduka ya kukodisha mikanda ya video, sheria hiyo imejikita zaidi katika utengenezaji wa filamu na maonyesho ya filamu hadharani (kwenye majumba ya sinema).

Kwa juhudi za Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na dhamira aliyokuwa nayo Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo kwa wakati huo, Mheshimiwa Kapteni Mstaafu George Mkuchika, wizara ikaanzisha mchakato wa marekebisho ya sheria hiyo iliyopitwa na wakati ili iwe SHERIA YA MAMLAKA YA FILAMU.

Huo ndiyo ulikuwa ufumbuzi wa kweli wa matatizo katika tasnia ya filamu.

Nini kilitokea?
Sisi kama wadau tuliitwa mwezi Mei, 2009 kujadili marekebisho ya sheria hiyo kwa siku mbili na kutoa mapendekezo yetu. Hatua iliyofuatia ilikuwa iwe ni majadiliano ya wadau wa ndani ya serikali kisha ipelekwe katika baraza la mawaziri kabla ya kupelekwa bungeni.

Pia siku ya tatu tulifanya uchaguzi wa kamati ya wadau kuangalia namna ya mchakato wa kuunda Shirikisho la Filamu Tanzania ili liweze kuwaunganisha wadau wa filamu kusukuma upatikanaji wa sheria hiyo.

Sitazungumzia mvurugano uliotokea kati ya BASATA, Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza pamoja na wasanii wa filamu kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa shirikisho kwa kuwa siyo muhimu kwa sasa kutokana na ukweli kuwa tayari kuna Shirikisho la Filamu Tanzania.

Ila kikubwa ninachokiona ni kuwa, kuna baadhi ya watendaji wa serikali wananufaika na mvurugano wa kisheria uliopo katika usimamizi wa tasnia ya filamu ndiyo maana wanakwamisha marekebisho ya sheria ya filamu na kuishauri serikali mambo ambayo hayawasaidii asilimia kubwa ya wadau wa filamu.

Waathirika ni kina nani?
Wasanii mastaa siyo waathirika sana wa hali iliyopo kwa maana huwa hawaigizi mpaka walipwe fedha wanazotaka, na hata wakiandaa filamu, wengi wao wanakuwa washauza haki miliki kwa wasambazaji ila wao ndiyo wanapata fursa ya kusikilizwa sana na viongozi wa juu wa serikali kwa kuwa ndiyo wanaoonekana sana kwenye vioo (screen). Siyo vibaya kutokana na uelewa wa viongozi wa juu kuhusu filamu ila je, wataalamu wa filamu walioajiriwa na serikali wanafanya nini?

Waathirika wakubwa ni watayarishaji waliowafanya hawa mastaa wawepo kisha wakawekwa pembeni na mfumo wa wasambazaji kuwapa hela moja kwa moja waigizaji wawatengenezee filamu ambazo wamiliki wanakuwa wasambazaji. Siwalaumu wasambazaji kwa sababu wanafanya biashara kutafuta faida, lawama ni kwa watendaji wa serikali ambao wanawafumba macho wasanii wasioelewa kuwa maadui zao ni wasambazaji kumbe wao ndiyo maadui.

Ukitaka kuuthibitisha ukweli huu kaangalie COSOTA kama kuna zaidi ya asilimia kumi za filamu za mastaa zinazomilikiwa na waliozitengeneza au ongea na watayarishaji wakongwe kama Amri Bawji wa Tanga, Sultani Tamba na Jimmy Mponda (Jimmy Master).

Waathirika wengine ni maelfu ya wasanii wachanga wanaohangaika kutoka na kuigizishwa kwa malipo kidogo katika filamu hizo za wasambazaji zinazotengenezwa na wasanii mastaa.

Hitimisho
Kutokana na hali hiyo nadhani mtakubaliana na mimi kuwa SERIKALI KUANZISHA STEMPU NI NJIA YA KUJIONGEZEA MAPATO YENYEWE NA SIO KUSADIA WASANII.

Sunday, April 8, 2012

UPEO!!!

Unapofikia kiwango cha juu cha kujitambua huwezi kushindwa kujibana hadi kufikia wembamba wa uzi ili tu upenye kwenye sindano kupata unachokihitaji. Wakati mwingine kuwa mjanja ni lazima uwe bwege! Ignas

USIPOTEZE!!!

Ukijua thamani ya kitu hutothubutu kukipoteza.
Lakini mara nyingi watu hugundua thamani ya wanavyovimiliki wakiwa wamechelewa sana na hawako navyo tena.
Zoea kutafakari kabla ya kutupa karatasi unalodhani ni uchafu, na hakika hutaweza kupoteza kitu cha thamani katika maisha yako.
Ni neno la hekima kwa waliobahatika kuwa na vichwa vya kuelewa mambo! Ignas

JIKUBALI!!!

USHAURI WA BURE! Ni vizuri ukiwa wewe na kuishi maisha yako kwa maana hakuna kama wewe katika dunia hii, ukijaribu kumuiga anayeishi maisha yake hakika maisha yatakushinda. Mwishowe utaombewa sana halafu utazidi kufua kwa kuwa hata Mungu ataona unamkera! Ignas